RAIS wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Patrice Motsepe, amesema hakuna mpango wa pili wala wa tatu wa kuhamishia AFCON 2027, akisisitiza kuwa Tanzania, Kenya na Uganda zitaendelea kushirikiana kuhakikisha maandalizi ya mashindano hayo yanakamilika kwa wakati.
Motsepe amesema amekuwa akipokea taarifa za maendeleo ya maandalizi na kwamba baadhi ya taarifa hasi zinazoripotiwa kwenye vyombo vya habari zinaweza kuwa za upotoshaji.

Amesema maeneo ambayo yameonekana kuwa nyuma katika maandalizi yataharakishwa na kurekebishwa, huku akieleza kuwa ana imani kubwa zaidi baada ya kupokea ripoti ya kina kuhusu maendeleo ya Tanzania.
Amesema anatarajia kurejea Tanzania Januari 2027 kwa ajili ya tathmini ya mwisho, kabla ya mashindano hayo kuanza Juni 19, 2027 hadi Julai 17, 2027.
Motsepe pia amesema atakwenda Kenya na Uganda kufuatilia maandalizi ya nchi hizo, akisisitiza kuwa CAF itashirikiana na waandaaji kuhakikisha changamoto zilizopo zinatatuliwa.
