SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imesema inapanga kutumia michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 kuwashawishi viongozi wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ili kuwapatia uwanachama kamili.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Habari, Sanaa na Utamaduni Zanzibar, Ali Abdulgulam Hussein, wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Ole, Seif Hamad Suleiman kwa niaba ya waziri wa wizara hiyo, Riziki Pembe Juma katika Baraza la Wawakilishi Chukwani, Unguja.

Ifahamike kwamba, wakati Zanzibar ikipambania hilo, kwa mujibu wa kanuni za sasa za CAF, uanachama ni wa chama cha taifa kinachowakilisha nchi inayotambuliwa kuwa huru na mwanachama wa Umoja wa Mataifa, na CAF inatambua shirikisho moja tu kwa kila nchi.
Zanzibar ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa mfumo wa FIFA na CAF, tayari kuna Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linalotambuliwa kimataifa, hivyo kutambua Zanzibar kama mwanachama kamili kupitia Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), kungeleta vyama viwili vya soka kutoka nchi moja.
Mwaka 2005, baada ya FIFA kukataa ombi la Zanzibar, iliondolewa CAF na baadaye ikarejeshwa kama mwanachama mshirika.
