Wakulima wa miwa katika Kata ya Bonga, Wilayani Babati mkoani Manyara, wameanza kuchangamkia fursa ya kilimo hicho kwa lengo la kuzalisha tani 800 ili kukabiliana na uhaba wa malighafi katika viwanda vya sukari mkoani humo.
Wakulima hao wameeleza matumaini yao ya kujikwamua kiuchumi kupitia mashamba makubwa waliyoanzisha, huku Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini, Mhe. Emmanuel Khambay, akiwatembelea na kuwataka waitumie vema fursa ya uwepo wa kiwanda cha Manyara Sugar kufanya kilimo chenye tija na endelevu.
Ili kuwapa uhakika wa soko, Afisa Kilimo wa Kata ya Bonga, Hamis Maganga, pamoja na Msimamizi Mkuu wa Shughuli za Kilimo kutoka kiwanda cha Manyara Sugar, Omary Hassan, wamethibitisha kuwa kiwanda hicho kiko tayari kununua miwa yote itakayozalishwa ili kukidhi mahitaji ya uzalishaji.
Hatua hiyo inalenga kuwahakikishia wakulima soko la uhakika na la haraka, sambamba na kuondoa changamoto ya upungufu wa sukari unaotokana na viwanda kukosa malighafi ya kutosha.
