Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Profesa Peter Msofe, ameipongeza Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) kwa hatua inazochukua kudhibiti uingizaji wa mbegu za mazao mbalimbali nchini bila kufuata taratibu na masharti yaliyowekwa.
Profesa Msofe ametoa pongezi hizo leo Oktoba 13, 2026, alipotembelea banda la TOSCI katika maadhimisho ya kitaifa kuelekea Siku ya Chakula Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, jijini Tanga.
Amesema ameridhishwa na mikakati inayotekelezwa na taasisi hiyo kuhakikisha mbegu zinazoingizwa nchini zinafuata taratibu na kukidhi viwango vilivyowekwa, akieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kulinda sekta ya kilimo na kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora.
Profesa Msofe pia amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa wadau mbalimbali, wakiwemo wasafirishaji wa mbegu, kuhusu taratibu za uingizaji na usafirishaji wa mbegu kutoka nje ya nchi.
Amesema elimu hiyo itasaidia kuongeza uelewa na kuzuia uingizaji holela wa mbegu ambao unaweza kuathiri uzalishaji wa mazao na maslahi ya wakulima.
Akitoa taarifa kwa Naibu Katibu Mkuu huyo wakati wa ziara yake katika banda la TOSCI, Mkaguzi wa Mbegu kutoka Kanda ya Kaskazini, Areth Kibaraza, amesema taasisi hiyo imefanikiwa kukamata basi lililokuwa likisafirisha mbegu katika eneo la Hololo, mkoani Kilimanjaro.
Kibaraza amesema katika kutekeleza jukumu hilo, TOSCI inashirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu (TPHPA) pamoja na Jeshi la Polisi, kuhakikisha mbegu zinazoingia nchini zinakidhi matakwa ya kisheria na taratibu zilizowekwa.
