Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeendelea kupanua wigo wa matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini, baada ya kuwezesha ujenzi wa miundombinu ya majiko ya kisasa na mifumo banifu mkoani Kagera, hatua inayolenga kulinda afya za wanafunzi na walimu pamoja na kutunza mazingira.
Uwekezaji huo umeshuhudiwa katika Shule ya Sekondari Ruhinda iliyopo wilayani Karagwe mkoani humo, ambapo takriban Sh milioni 60 zimetumika kukamilisha ujenzi wa jengo jipya la jiko la kisasa; usimikaji wa mifumo ya nishati safi ya kupikia pamoja na ununuzi wa tani 13 za kuni mbadala (kuni poa).
Akizungumza baada ya kutembelea shule hiyo Oktoba 12, 2026, Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Mbadala na Jadidifu kutoka REA, Mhandisi Advera Mwijage, alisema mradi huo umetekelezwa kupitia mkataba wa ruzuku uliosainiwa Agosti 20, 2026 kati ya REA na Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe ambao ndio walikuwa waratibu wa ujenzi huo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Ruhinda, Ambruse Abel, ameishukuru REA na serikali kwa ujumla akieleza kuwa mradi huo umekuwa chachu ya kuongeza ufaulu kwa wanafunzi takribani 700 wanaosoma shuleni hapo.
