Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za tahadhari na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu ugonjwa wa Ebola ili kuzuia uwezekano wa kusambaa kwa ugonjwa huo nchini.
Akijibu maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu Bungeni jijini Dodoma leo Juni 4, 2026, Dkt. Mwigulu amesema Tanzania si kisiwa, na ina mahusiano ya kijamii, kiuchumi na kiutamaduni na mataifa jirani, hali inayosababisha watu kuvuka mipaka mara kwa mara, hivyo kuongeza umuhimu wa kuwa makini dhidi ya magonjwa ya mlipuko.
Amesema Serikali imeendelea kuhamasisha wananchi kuchukua tahadhari zote muhimu pamoja na kutumia majukwaa mbalimbali kutoa elimu kuhusu namna ya kujikinga na Ebola, akibainisha kuwa ugonjwa huo si mpya katika ukanda huo.
Dkt. Mwigulu ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kuelimishana na kuripoti mapema dalili zozote zinazoweza kuashiria maambukizi ya Ebola ili wahusika wapatiwe huduma za haraka na kuzuia kuenea kwa maambukizi.
Amesisitiza umuhimu wa watu wanaoingia nchini kutoka nje kufanyiwa uchunguzi wa afya na kutoa taarifa sahihi bila kuficha dalili, akisema ushirikiano wa wananchi ni nguzo muhimu katika kudhibiti magonjwa ya mlipuko.
