Kongamano la Sita la Kitaifa la Utoto Mtakatifu lililokuwa lifanyike kuanzia Juni 18 hadi 22 mwaka huu katika Jimbo Katoliki la Kigoma limeahirishwa hadi hapo tarehe mpya itakapotangazwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).
Taarifa ya kuahirishwa kwa kongamano hilo imetolewa na Ofisi ya Mashirika ya Kipapa Taifa, ikieleza kuwa uamuzi huo umetokana na tafakari ya kina iliyofanywa na Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini baada ya kusoma alama za nyakati na kuzingatia masuala yaliyo nje ya uwezo wao.
Kongamano hilo lilitarajiwa kuwakutanisha watoto kutoka majimbo mbalimbali nchini kwa lengo la kuimarisha malezi ya kiroho, kukuza ari ya kimisionari na kuwajengea watoto utamaduni wa huruma, upendo na mshikamano kwa wenzao wanaoishi katika mazingira magumu.
Shirika la Utoto Mtakatifu ambalo ndilo mwandaaji wa kongamano hilo, lilianzishwa mwaka 1843 kwa lengo la kuwahamasisha watoto kushiriki katika kusaidia watoto wenzao wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo umaskini, magonjwa, njaa na ukosefu wa elimu.
Ofisi ya Mashirika ya Kipapa Taifa imewaomba waamini na washiriki kupokea mabadiliko hayo kwa utulivu, ikisisitiza kuwa hatua hiyo imechukuliwa kwa kuzingatia maslahi mapana ya watoto na Kanisa kwa ujumla wake.
Wakati huo huo, ofisi hiyo imewahakikishia washiriki wote waliokwisha kuwasilisha michango ya ushiriki kuwa fedha hizo ziko salama na zitaendelea kuhifadhiwa hadi hapo tarehe mpya ya kongamano hilo itakapotangazwa rasmi na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.
