Rais wa Zanzibar Dk.Hussein Ali Mwinyi amezindua usafiri wa umma wa mabasi ya umeme na Kituo cha Mabasi cha Malindi, ikiwa ni kuboresha mfumo wa usafiri na kuhamasisha matumizi ya nishati safi visiwani humo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Dkt. Mwinyi ameitaka Zanzibar Social Security Fund (ZSSF) kuharakisha ujenzi wa vituo vya kisasa vya mabasi ili wananchi waweze kunufaika kikamilifu na huduma hiyo.
Amesema mradi wa mabasi ya umeme utachangia kuboresha usafiri wa umma, kupunguza uchafuzi wa mazingira na kuimarisha matumizi ya nishati mbadala.
Aidha, amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa barabara, maji safi, bandari, viwanja vya ndege, hospitali na miundombinu ya Michezo.
