Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padre Dkt. Charles Kitima, amesisitiza kuwa mkwamo wa kisiasa nchini utatatuliwa tu ikiwa kutakuwa na utayari wa kukiri makosa, kusimamia ukweli, na kuombana msamaha kufuatia matukio yaliyogubika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025
Akizungumza na waandishi wa habari leo , kufuatia mkutano kati ya TEC na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan uliofanyika Ikulu ya Chamwino tarehe 10 Agosti, Padre Kitima amebainisha kuwa msingi wa andiko walilomkabidhi Rais ni kuhakikisha nchi inapata uponyaji wa kweli.
Padre Kitima ameeleza kuwa viongozi wa kiroho wanaona kuna haja ya kuwa na ujasiri wa kutaja kile kilichokwenda mrama ili kurejesha mahusiano yaliyovunjika kati ya serikali na wananchi. Amebainisha kuwa bila kukiri ukweli wa yaliyotokea, mchakato wa maridhiano hautakuwa na tija
“Kutokana pia na kwamba waliweka bayana kwamba ili tutoke katika hali hii inabidi kwenda katika kusimamia ukweli na vile vile kutakana msamaha kusameheana na hata kuponya nchi. Kwa hiyo kwa kiingereza tunasema ‘to admit the truth then reconciliation healing the nation’,” amesisitiza Padre Kitima
Katibu Mkuu huyo amekiri kuwa matukio ya tarehe 29 Oktoba 2025 yameacha sononeko kubwa kwa Watanzania wengi na kuharibu imani ya raia kwa mamlaka zao. Amesisitiza kuwa maaskofu wameweka wazi masikitiko yao kuhusu mauaji na uharibifu wa mali uliotokea na kwamba sasa ni wakati wa kutatua mambo hayo yaliyosababisha watu kuingia katika hali ya maandamano
