Samwel Masunzu- Kibondo, KIGOMA
KIBONDO: Askofu wa Kanisa la Free Pentecostal Church FPCT wilayani Kibondo Mkoani Kigoma Meshack Christopher amezindua mradi wa Tustahimili ambao unasimamiwa na kanisa hilo ukilenga kutoa elimu kwa wananchi wa dini zote juu ya kuongeza kipato na kutunza mazingira.
Askofu Christopher kupitia uzinduzi huo katika ukumbi wa chama cha walimu CWT wilayani humo amewataka walengwa wa mradi huo kuhakikisha wanashirikiana kwa pamoja katika shughuli zao na kufanya kazi kwa bidii na kwa uaminifu nakwamba lengo la kanisa ni kuikutanisha jamii kutoka dini zote na kuijengea uwezo wa kufanya shughuli za kiuchumi zenye kuwaletea tija.

Awali mratibu wa mradi huo Bw. Leopold Muhagaze amesema mradi huo unatakelezwa katika kipindi cha miaka 3 kuanzia mwaka huu 2026 hadi Disemba 2028.
Muhagaze amesema lengo kubwa la mradi huo ni kutoa elimu ya jamii kutambua umuhimu wa kutunza mazingira kupitia upandaji wa miti, kuanzisha, kurasimisha na kuendeleza biashara na walengwa ni vijana, wanawake na wanaume wenye umri kuanzia miaka 18 – 45 na utagharimu kiasi cha shilingi milioni 110.
Afisa maendeleo ya jamii kutoka halmashauri ya wilaya ya Kibondo Bw. Paschal Msoffe pamoja na afisa maendeleo ya jamii kata ya Kibondo mjini Bi. Jackline Isaack wamesema serikali inatoa mikopo isiyo na riba kwa lengo la kuwainua wananchi kiuchumi, hivyo wanapaswa kuunda vikundi ambavyo vitawasaidia katika kupata mikopo hiyo.

Baadhi ya washiriki katika uzinduzi huo Bi. Spesioza Gwimo na Bw. Sultan Maguru Wamesema mradi huu utawasaidia katika kuendeleza shughuli za ujasiliamali na kupata muunganiko sahihi kati yao na maafisa kutoka halmashauri juu ya taratibu za kupata mkopo na kurejesha kwa wakati.
