Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limesisitiza kuwa mazingira safi na salama ni msingi wa maendeleo endelevu ya Uchumi wa Buluu, unaotegemea rasilimali za bahari, mito, maziwa na maeneo ya pwani.
NEMC imesema uhifadhi wa mazingira haupaswi kuonekana kama kikwazo cha shughuli za kiuchumi, bali ni sehemu muhimu ya kuhakikisha rasilimali hizo zinaendelea kutoa ajira, chakula, mapato na fursa za uwekezaji kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Kauli hiyo imetolewa wakati wa Kongamano la 5 la Kimataifa la Uchumi wa Buluu, linalofanyika chini ya kaulimbiu “Powering Blue Initiatives for Sustainable Economic Growth in Africa”.
Katika kongamano hilo, NEMC imeeleza kuwa inaendelea kutekeleza wajibu wake kupitia Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA), ukaguzi, ufuatiliaji wa uzingatiaji wa masharti ya mazingira na udhibiti wa uchafuzi.
Baraza pia limeelezwa kuwa uchafuzi wa bahari, taka za plastiki na uharibifu wa mifumo ikolojia ya maeneo ya pwani ni miongoni mwa changamoto zinazoweza kudhoofisha manufaa ya Uchumi wa Buluu endapo hazitadhibitiwa.
Kongamano hilo lilifunguliwa rasmi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yusuf Masauni, kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi.
NEMC imesisitiza kuwa matumizi endelevu ya rasilimali za majini yanahitaji uwiano kati ya shughuli za kiuchumi na uhifadhi wa mazingira ili kuhakikisha Uchumi wa Buluu unakuwa na manufaa ya muda mrefu.
