Na Enock Yoronimo- Bukoba, KAGERA
Serikali kupitia Bodi ya Kahawa Tanzania imesema ina mpango wa kuongeza uzalishaji wa miche ya kahawa kwa kuzalisha miche milioni 30 kwa mwaka 2026/2027 ili kuhakikisha wakulima wanapata miche bora.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Kahawa Tanzania, Prof. Aurelia Kamuzora, akiwa ziarani mkoani Kagera kwa lengo la kuhamasisha kilimo cha kahawa yenye ubora wa kimataifa.

Prof. Kamuzora amesema zaidi ya miche bora ya kahawa milioni 20 hadi 22 imezalishwa na kugawiwa kwa wakulima nchini ikiwa ni jitihada za kuongeza uzalishaji wa zao hilo pamoja na kukuza uchumi wa wananchi wanaotegemea kilimo cha kahawa.
Meneja wa Bodi ya Kahawa (TCB) mkoa wa Kagera Edmond Zani amesema miche milioni 13 iligawiwa kwa wakulima katika msimu uliopita na kuzalisha tani milioni 50 hadi 80 za kahawa kwa mwaka, jambo linaloufanya mkoa huo kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa zao hilo nchini.
Aidha Wajumbe hao wa bodi ya kahawa mkoni Kagera wametembelea kiwanda cha kuchakata kahawa cha Amimza kilichopo Bukoba, kitalu cha uzalishaji wa miche bora ya kahawa cha JADI, shamba la vijana la heka 300 Makongora pamoja na kiwanda cha Kyeju na shamba la kahawa wilayani Muleba mkoani humo.

