
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknojia (Costech), Dk Amos Nungu katika picha
Tanzania imepiga hatua ya kuchukua teknolojia zilizokwisha muda wa umiliki katika nchi nyingine ili kuja kusaidia jamii katika maeneo ya uzalishaji ili kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kiujumla.
Hatua hiyo inafuatia ushirikiano na Shirika la Miliki Ubunifu Duniani (WIPO), ambapo utekelezaji umeanza kupitia mradi wa kwanza wa teknolojia ya kilimo na ufugaji mkoani Njombe.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa mradi huo uliofanyika Dar es Salaam leo Jumatatu, Juni 1, 2026, Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Dk Amos Nungu amesema wanaangalia kwenye kanzi data ya WIPO, teknolojia sahihi kwa ajili ya mazingira ya Tanzania.
Mkuu wa Kitengo cha Uratibu wa Nchi Zinazoendelea Kidogo, Nchi Zisizozungukwa na Bahari na Nchi Ndogo za Visiwani katika shirika la WIPO, Purevdorj Vaanchig amesema uzinduzi wake una lengo la kujenga uwezo, hasa wa kiteknolojia wa vyuo vikuu vya ndani na taasisi za utafiti,ikiwa ni kuja kusaidia jamii za ndani na kuboresha maisha ya wananchi. Sehemu ya pili ya mradi ni kujenga ujuzi ndani ya vyuo vikuu na kuchangia katika mfumo wa ikolojia wa ubunifu wa ndani.
Awali, Mkurugenzi wa Miliki Ubunifu kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) Loy Mhando, amesema WIPO walikubali kuipa Tanzania teknolojia sahihi kwa ajili ya kusaidia maendeleo ya jamii.
Mkurugenzi wa Utafiti na Ubunifu kutoka Taasisi ya Nelson Mandela,Profesa Thomas Kivevele, amesema wakiwa kama wadau wa mradi huo watakuwa wanachakata taarifa zinazotoka kwenye chanzo ili kuja na ubunifu utakaotatua changamoto ya chakula cha mifugo.
