Rais Samia Suluhu Hassan, amewataka majaji wapya wa Mahakama ya Rufani kutenda haki kwa uadilifu, weledi na bila upendeleo ili kuimarisha amani, utulivu na maendeleo ya taifa.
Akizungumza baada ya kuwaapisha majaji hao leo Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Samia alisema haki ndiyo msingi mkuu wa ustawi wa taifa na wananchi wake.
“Nendeni mkaitumikie nchi kwa uadilifu, weledi na uzalendo… mfanye kazi bila upendeleo, huba wala chuki,” amesema Rais Samia.
Aidha amewataka majaji hao kutambua uzito wa dhamana waliyopewa ya kusimamia haki za wananchi pamoja na maslahi ya taifa kupitia maamuzi yao ya kimahakama.

Rais Samia amesema kazi ya utoaji haki ni wajibu mkubwa unaohusiana m kwa moja na huduma kwa jamii na mbele ya Mungu.
“Wale ambao Mungu amewateua kusimamia haki za wenzao ni nyinyi majaji katika ngazi zenu tofauti,” amesema.
Aidha, amesisitiza kuwa majaji wanapaswa kufanya maamuzi kwa kuzingatia sheria, haki na maslahi ya wananchi bila kuathiriwa na hisia binafsi.
