Kundi la wafugaji wa Kijiji cha Losirwa kilichopo Kata ya Esilalei, Wilaya ya Monduli mkoani Arusha, wamekusanyika na kukesha porini kwa siku tatu mfululizo kulalamikia uongozi wa kijiji chao kwa tuhuma za kuuza ardhi ya nyanda za malisho.
Wakazi hao, wakiwemo Masiaya Kimiti na Mery Sangeti, wameeleza kuwa wamelazimika kuchukua hatua hiyo ili kupaza sauti zao na kuzuia uuzaji wa eneo hilo ambalo ndilo tegemeo kuu kwa ajili ya usalama wa mifugo yao.
Kufuatia sakata hilo, Mwenyekiti wa Kijiiji cha Losirwa, Yamat Lucas, amekanusha vikali kuhusika na uuzaji huo, huku Mwenyekiti wa Halmashauri ya Monduli, Kisiok Moitiko, akisisitiza msimamo wa kulinda maeneo ya umma na kufuata sheria.
Mbunge wa Jimbo la Monduli, Isaac Joseph, amefika katika eneo la tukio kusikiliza pande zote mbili na kutoa maonyo makali kwa wale wote wanaojihusisha na njama za kuwadhulumu wafugaji hao maeneo yao ya malisho.
