Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba amesema wahasibu, wakaguzi wa hesabu na washauri elekezi wa masuala ya kifedha wana nafasi kubwa katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kupitia usimamizi bora wa fedha, uwajibikaji na matumizi salama ya mifumo ya kidijitali katika sekta ya fedha.
Amesema licha ya changamoto za uchumi duniani, Tanzania imeendelea kuwa miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri kiuchumi huku sekta ya fedha ikiendelea kuwa himilivu.
Tutuba amesema hayo leo Jumatatu Mei 25, 2026 jijini Arusha wakati akifungua semina ya pamoja kati ya Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) na BoT iliyolenga kujadili namna ya kuimarisha mfumo wa fedha endelevu kwa kutumia teknolojia pamoja na kuzingatia misingi ya utawala bora katika sekta ya fedha na uhasibu.
Aidha, amesisitiza matumizi ya mifumo ya kidijitali katika miamala ya kifedha badala ya kutegemea fedha taslimu ambazo zina vihatarishi mbalimbali.
Mkurugenzi Mtendaji wa National Board of Accountants and Auditors, Siasa Mzenzi amesema semina hiyo imejikita katika kujadili uendelevu wa sekta ya fedha pamoja na matumizi ya teknolojia katika usimamizi wa fedha.
