Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeanza kutekeleza maelekezo ya Wizara ya Nishati kwa kufunga transfoma mpya kubwa katika Wilaya ya Ngara mkoani Kagera.
Hatua hiyo inalenga kuboresha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wananchi kufuatia agizo la Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi kwa TANESCO kuhakikisha inapeleka na kufunga transfoma mpya ndani ya muda mfupi kufuatia changamoto ya kukatika kwa umeme iliyokuwa ikilalamikiwa na wananchi wa eneo hilo.
Kwa mujibu wa taarifa, transfoma hiyo yenye uwezo wa 5MVA imewasili katika kituo cha kupozea umeme cha Djululigwa wilayani Ngara, ambapo wataalamu wa TANESCO wameanza kazi ya ufungaji.
Meneja wa TANESCO Wilaya ya Ngara, Mhandisi Amani Chidundo, amethibitisha kuwasili kwa transfoma hiyo na kueleza kuwa kazi ya kuifunga imechukua takribani saa 12 kukamilika.

Amesema changamoto ya umeme katika wilaya hiyo ilichangiwa na transfoma ya awali yenye uwezo wa 3MVA kuzidiwa na ongezeko la matumizi ya umeme, hali iliyopelekea kushuka kwa ufanisi wa huduma.
Kwa upande wake, Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Ngara Soud Mukubila ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Nishati na TANESCO kwa hatua ya haraka ya kushughulikia changamoto hiyo, akisema itasaidia kuboresha huduma kwa wananchi.
