Imeelezwa kuwa mfumo wa elimu ya watu wazima mkoani Kagera unakabiliwa na changamoto ya mwamko duni wa vijana kutojiunga na mfumo huo licha ya serikali kuwahamasisha waliokosa elimu ya mfumo rasmi kujiunga katika elimu ya watu wazima.
Afisa elimu ya watu wazima wilaya ya Karagwe Willison Byarugaba ameeleza hayo septemba 16,2026 wakati akisoma risala kwenye maadhimisho ya Kisomo na kilele cha juma la elimu ya watu wazima kimkoa yaliyofanyika uwanja wa posta Ngara mjini.
Aidha Bw. Byarugaba amesema mfumo wa elimu ya watu wazima inakabiliwa na changamoto ya vituo kukosa vitendea kazi vya kutosha kwa ajili ya kufundishia na kujifunzia elimu ya ufundi.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo Mkuu wa wilaya ya Biharamulo SACP. Advela Bulimba akimwakilisha mkuu wa mkoa wa Kagera amewaagiza watendaji wa sekta ya elimu mkoa kufuatilia asilimia 3.3 ya watu wasiojua kusoma na kuandika ili watengenezewe program maalum inayoendana na mahitaji yao ya kujifunza.

